<< The Mirror Translation >>
WARUMI WALIFUNULIWA |
|
WARUMI WALIFUNULIWA
Injili ya Paulo iliyositirika
Tafsiri kutoka maandishi ya asili na: Francois du Toit
UTANGULIZI
Tai huru
Tulipokuwa katika muda wa mapumziko ya arusi yetu (fungate) kule Blydepoort, Mpumalanga (Jan 1979) Lydia na mimi tulikutana na afisa wa kike kutoka hifadhi ya mali asili aliyetuambia juu ya tukio lililohusu ukamataji. Alitushuhudia hadithi ya kuachiliwa kwa Tai Mweusi majuma machache kabla ya ziara yetu. Tai huyu alikuwa mateka katika bustani ya Pretoria kwa miaka kumi.
Alitueleza jinsi walivyosisimliwa kwa furaha na matazamio makubwa wakati tai alifika akiwa tunduni mwake, na hatimaye kilango kufunguliwa. Lakini walifanikiwa kumtoa ndege yule kutoka tundu lake kwa shida kubwa.
Lilikuwa ni jambo moja kumtoa ndege tunduni; lakini ni jinsi gani unalitoa tundu kutoka ndani ya ndege? Katika akili ya tai huyu, alikuwa bado ni mfungwa ndani ya bustani!
Kila mmoja alivuta pumzi, lakini ndege huyu mwenye nguvu alibakia kuwa mfungwa wa kuhurumiwa kwa kuwa na akili duni.
Hakuna kilichobadilika mpaka baadaye wakati tai mwingine alipoanza kuita katika eneo lile. Macho ya tai wa hifadhini mara yalifunguka, na kufuatiwa na na kuruka kwa mruko wa utukufu, kuruka katika nafasi isiyozuilika. Hayakuhitajika maelekezo zaidi namna ya kuruka!
Hadithi hii iliacha mguso mkubwa katika akili yangu. Nilijua kuwa, kufuatana na ufunuo wa Paulo kuhusu habari njema, tumeachiwa jambo la kipaumbele, ambalo ni kutangaza kwa mataifa kwa ujasiri mkubwa, ukweli kuhusu utambulisho wao wa asili, na kuakisi kwa kioo, uadilifu wao wa kutokuwa na hatia.
Injili ya Paulo
Katika barua yake kwa Warumi, Paulo anatoa mambo ya awali na haraka yaipasayo Injili ya Yesu Kristo katika mtindo tofauti kabisa.
Katika kujifunza kitabu hiki kilicho kiini cha Biblia, utaanza kuelewa kwa nini Paulo aliinena Injili yake kwa msisitizo mkubwa.
Anaondoa kila uongo ambao labda mtu aliweza kuongeza au kutoa kutoka katika ufunuo huu. Inahusisha jumla ya ustawi wa wanadamu duniani; jinsi Muumbaji alivyoweza kukomboa na kurejesha sura na mfano wake katika umbo la kibinadamu.
Paulo ameshawishika kuwa, lolote lililotokea kwa taifa la wanadamu kwa sababu ya anguko la Adamu, lilibatilishwa kwa kadiri iwezekanavyo na ufunuo wa kuunganishwa kwa mtu katika uzima, kifo na ufufuo wa Yesu kristo.
Analiweka anguko la Adamu na kila tendo lisilo la haki ambalo lilifuata dhidi ya tendo moja la haki ambalo Mungu alilifanya katika Kristo kama achilio la mwisho la mwanadamu.
Kila fundisho ambalo bado linaweka msisitizo juu ya mchango wa mtu sawasawa na amri na sheria zilizoagizwa ili kujiridhisha mwenyewe na mwenendo wake, linamzuia tena mtu kwa nidhamu binafsi na juhudi chini ya mfumo duni wa sheria ya hatia na hukumu; na kudharau kazi iliyokamilishwa na Mungu katika Kristo.
“Hata chachu kidogo huchachusha donge zima” ndivyo asemavyo katika barua yake kwa Wagalatia. (5:9)
Ufunuo wa haki kwa imani unafungua jinsi Mungu, ndani ya Kristo, alivyoweza kurejesha hali kutambuliwa kwa mtu, na hali ya kuwa bila hatia iliyopotea. Uhalisi wa maana ya neno, ‘haki’ katika chimbuko lake, dike, lina maana ya wazo la sehemu mbili zinazotafuta kufanana kila moja kwa nyingine; bila mwingiliano wowote wa hali ya lawama, hatia na kujiona duni.
Katika nyaraka zake Paulo anatangaza kwa usemi usio na shaka kwamba, hakufanya juhudi yoyote kujifunza au kuazima ufunuo wake wa Injili kutoka kwa wanafunzi wa Yesu kumi na mmoja wa kwanza.
“Kwa maana, ndugu zangu, Injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri mataifa habari zake, mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu.” Gal. 1:11,12,15-17.”
Mtu angeweza kufikiri kuwa Paulo alikosa fursa muhimu mara baada kuokoka kwake, kwa kuwa hakujifunza kwa mara ya kwanza kwa kirefu taarifa ya ushuhuda wa macho, ambao mitume walitakiwa kumpa kuhusu Yesu wa Nazarethi.
Lakini mguso alioupata, ulimweka mbali na thamani aliyokuwa nayo hapo kwanza kutokana na uzao wake wa kiungwana. Chochote alichokipata alihisi kuwa alikipata kwa sababu alikuwa ni wa jamaa ya ukoo uliotukuka wa Benyamini. Hali hii ilimpunguzia ufunuo mkuu jinsi ya kutambuliwa kwa mtu. “Hata imekuwa,sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili…” (2Kor.5:16.) “Hapana Myahudi wala Myunani, Hapana mtumwa wala huru, hapana Mwafrika wala Mchina, hakuna mtu mume wala mke…” (Gal.3:28.)
Hakuna kinachomtofautisha mtu zaidi kuliko ufunuo wa kutambuliwa kwake kwa asili kama kulivyotunzwa, kurejeshwa na kufunuliwa tena katika Kristo.
Katika Kristo sura na mfano wa Muumba asiyeonekana umeonekana kiusahihi katika umbo la mwanadamu. “Ni katika yeye Mungu anatoa udhihirisho wake mwenyewe ulio mtimilifu na mkamilifu. Zaidi ya hayo, ukamilifu wako umefunuliwa katika yeye tu.” (Kol.1:15; 2:9.10. Tafsiri ya Phillips).
Paulo aliwakumbusha wasomi wa Athene kuwa, “Hayuko mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda na kuwa na uhai wetu. Maana sisi sote tu wazao wake...” (Mdo17:27,28.) Kioo cha ndani cha Kristo kinasema yote! Kufanana kwetu na Kristo kulikofunuliwa ndani yetu kunaleta mabadiliko ya kweli; utambuzi huu una matokeo zaidi kuliko kufikiria mema tu, ‘ni kama kuangalia mali dirishani tu, bila kununua’ au kutumia nguvu za matakwa yetu! (2Kor.3:18.)
Hakuna hata mara moja katika Nyaraka zake Paulo, mahali anapotaja muujiza wowote uliofanywa na Yesu, wala kutolea mfano wowote ulionenwa na Yesu.
Utume wake na ujumbe haukuwa kumtangaza Kristo aliyefunuliwa katika historia, bali Kristo aliyefunuliwa ndani yetu! (Rum.8:10). Anasherehekea mavuno yaliyofunuliwa katika chembe moja ya ngano ambayo ingekuwa imebakia peke yake, kama isingekuwa imepandwa ardhini na kufa (Yoh. 12:23,24).
Siri iliyositirika tangu vizazi vyote vya watu, haikujulikana na mtawala yeyote wa dunia hii. Mungu aliionyesha siri hii ndani ya kufanyika mwili kwa Yesu, kwa ajili ya utukufu wa mwanadamu. “Wangeliijua wasingalimsulubisha Bwana wa utukufu.” (1Kor.2:6-9.) Lakini hawakuijua siri ya mpango wa Mungu, jinsi mwanadamu alivyotakiwa kuwakilishwa na kuunganishwa katika Kristo; jinsi ambavyo mmoja angekufa kwa ajili ya wote, na jinsi ambavyo mara moja wote walikufa katika kifo chake. (2Kor.5:14.) Hawakujua kwamba wanadamu wote wangewakilishwa katika tendo moja la mtu mmoja, hivyo kuyaondoa madai ya giza na ujinga juu ya watu wote. “Mungu alijifanya kama hazioni zamani za ujinga.” (Mdo 17:30). Historia iliandika kifo na ufufuo wa mmoja, milele iliandika kifo cha wanadamu na uzao mpya wa jamii za wanadamu.
Kwa ujinga wetu wenyewe, tulimpa shetani manufaa makubwa; lakini ameshindwa na kuondolewa! Katika ufunuo wa Injili amefanyika kuwa si kitu na kutokuwa na nguvu kabisa! (1Kor.2:6-8; Kol.2:14,15) Kusudi lake pekee daima limekuwa kumfanya mwanadamu adumu kuwa mjinga kama yeye mwenyewe alivyokuwa, wasijue kuhusu kuunganishwa kwao ndani ya Kristo. Ulikuwa ujinga wetu na kutokuamini kwetu kulikompa nguvu za kufanya hivyo.
Andiko pekee katika Agano la kale juu ya kufufuka siku ya tatu kwa kutujumlisha na sisi pia ni, “Siku ya tatu atatuinua!” (Hos.6:1,2). Hili ni andiko lililochochea ufahamu wa Paulo kwamba sisi sote tulijumlishwa katika kifo chake na ufufuo wake wa ushindi. Ni masharti ya nani yaliwafanya walistahili kuunganishwa? “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu” ndivyo asemavyo Paulo katika 2Kor.5:18. “Bali kwa Mungu ninyi mmepata kuwa katika Kristo.” (1Kor.1:30) “Miisho ya dunia katika vizazi vitakavyokuja watajua kuwa ndiye Bwana aliyeyafanya!” (Zab.22:31) Haya yalitimizwa kwa niaba yetu tulipokuwa tungali wafu katika dhambi zetu; tulipokuwa adui na duni kumwelekea Mungu. (Ef.2:5,6). Kwa sababu tulifufuliwa pamoja na Kristo, na tushikwe na hali ya kushughulika na mawazo pamoja na kweli za chumba cha enzi, na wala sio migongano isiyo na maana wala uzima. (Kol.3:1-3).
Baada ya kukaa miaka mitatu katika ukiwa kule Arabia, Paulo alitembelea Yerusalemu kwa majuma mawili, na kwa kuangalia, aliwaona wanafunzi wawili tu, Kefa na Yakobo ndugu yake Bwana. Ni nini kilichowatofautisha Petro na Yakobo ndugu mdogo wa Yesu, na wanafunzi wengine? Kwa nini hasa Paulo alivutwa nao? Watu hawa wote walishiriki kidogo ufunuo pamoja na Paulo; hawakumjua tena Yesu katika hali ya mwili; walikuwa wamegundua utambulisho wao wa kweli katika Kristo.
Paulo anamtaja Petro kama Kefa ili kusisitiza maana kuliko kusikika kwa jina lake kulikozoeleka! Katika Kigriki, lugha ya kuandikwa ya siku zile, neno ‘mwamba’ lilikuwa “petros,” lakini kwa lugha ya kuzungumza ambayo ilikuwa kiaramu neno lilikuwa “Kefa.”
Katika Mathayo 16 Yesu anauliza swali muhimu sana katika Biblia, “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” Kwa ufunuo, Simoni anathibitisha kwa kujibu kuwa Yesu si Mwana wa Yusufu, bali Yesu ni Masihi. Yeye ni ahadi ya ukombozi wa wanadamu, sura na mfano wa Mungu uliorejeshwa na kuonekana kikamilifu katika umbo la kibinadamu; Mwana wa Mungu aliye hai.
Angalia jinsi Yesu anavyomjibu, “Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.” Ikiwa mimi ni Mwana wa Mungu, basi pia na ninyi! Jina lako la ukoo halitokani tena na baba yako wa kawaida katika mwili , bali kutoka katika Mwamba uliokuzaa! (Kumb.32:18, “Uangalieni mwamba ule ambao mlitolewa kwa kuchongwa.” Is.51:1) “Juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu.” Kigriki ni ekklesia.
Kanisa ni jibu la Mungu kwa utambulisho wa mwanadamu uliopotea. Neno ‘ekklesia’ lililotajwa na Yesu hapa, halimaanishi jengo au shirika, bali utambulisho wa kwanza ki-Mungu wa mwanadamu uliorejeshwa na kufunuliwa upya katika Kristo kama vile kwa kioo. Kitangulizi cha Kigriki, ek, daima humaanisha chanzo au chimbuko, (1Kor.1:30; Ebr.2:11) na klesia, kutoka kaleo, maana yake kumtaja ukoo au kumtambua kwa jina. Maana muhimu na kusudi la kanisa ni kueneza huduma ya Yesu Kristo, ambayo ni kufunua utambulisho wa kweli wa kila mtu kufanana na Kristo. “Alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu.” (1Pet.1:3).
Nyongeza kwa Petro, je, Paulo pia alimtembelea Yakobo? (Gal. 1:19). Je, ni nini kilichomtokea Yakobo kwa kujitenga na kutokujali huduma ya ndugu yake Yesu? (“Maana hata nduguze hawakumwamini” Yoh.7:5). Ni nini kilichomfanya kuandika kwamba uzao wetu ni wa Baba wa mianga, aliyetuzaa sisi kwa neno la kweli? Mwanzo wetu wa kweli uko katika Mungu; sisi ni uvumbuzi wa Mungu. “Na kila asikiaye neno hili, hujiangalia uso wa kuzaliwa kwake kama katika kioo.” Pia anaeleza inawezekana kusahau kuwa wewe ni mtu wa namna gani, ikiwa utakuwa umevutwa kutoka katika mtazamo wa imani katika kioo wa kufanana naye, na kurudi tena katika mawazo ya nia mbili ya mwili. (Yak.1:17,18,24)
Katika 1Kor.15:7, Paulo anatamka wazi kuwa, pia Yesu alimtokea Yakobo baada ya ufufuo. Ninaamini kuwa maana ya huduma ya Yesu ilikuwa imepambazuka ndani yake. Sasa, alijua kuwa ndugu yake alikuwa ni Masihi kweli kweli. Mara alielewa kuwa sawa sawa na Yesu, mwanzo wake pia ulianza katika Mungu; kama ilivyo uzao wa kweli wa mtu, sasa umewakilishwa na kufunuliwa katika ufufuo. Yusufu na Mariamu hawakuwa wazazi wa mwanzo wa asili ya roho.
Paulo alishawishika kuwa kuna jambo lilitokea kwa mwanadamu katika kifo na ufufuo wa Kristo. Ufufuo unaakisi uzao mpya wa kila mtu. Hili lilitokea hata kabla sisi hatulijui. “Hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja naye.” (Ef.2:5) Paulo alipohubiri ufufuo katika Matendo ya mitume 13, alitumia Zaburi 2 kama msingi, “Mimi leo nimekuzaa.” (Mdo 13:30-33)
“Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.” (1Kor.15:22). Yesu hakuwa Adamu wa pili, bali Adamu wa mwisho. Mambo ya kwanza, (kizazi cha Adamu wa kale) yamepita. “Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha.” (1Kor.15:45)
“Maana tumehukumu hivi, ya kwamba, mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote. Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya.” (2Kor.5:14,16,17)
Je, wanadamu wote walikufa lini? Kulingana na sababu za Paulo, hili lilitokea wakati Yesu alipokufa. Yesu katika nafsi yake aliwakilisha mambo ya Mungu yote katika umbo la kibinadamu, na wakati ule ule, mambo yote ya wanadamu.
Yesu hakuja kuanzisha dini ya kikristo; alikuja kufunua asili ya kweli wa kila mtu, utambulisho wake, na kuwa bila hatia. Injili ilipohubiriwa kwa Wayunani kwa mara ya kwanza, Barnaba alitumwa na kanisa la Yerusalemu ili kuchunguza taarifa. Aliona neema na ushuhuda ndani yao, na badala ya kurudisha taarifa kwa uongozi wa Yerusalemu, mara alimtwaa Paulo na kumpa nafasi ya kuhubiri hadharani. Alijua na kuelewa ufunuo wa Paulo kuhusu Kristo ndani ya mwanadamu. Si ajabu tukijifunza kuwa, kulikuwa ni Antiokia ambako mara ya kwanza waamini waliitwa Wakristo. (Mdo 11).
“Uniombe nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, na miisho ya dunia kuwa milki yako!” (Zab.2:7,8). Kukamilika kwa kazi ya msalaba ni kwamba, miisho ya dunia yote itakumbuka (utambulisho wao uliosahauliwa. Kumb.32:18), na kumgeukia Bwana. (Zab.22:27).
“Namhubiri Yesu Kristo sawasawa na ufunuo wa siri iliyositirika katika ukimya tangu milele, bali sasa imejulikana wazi, imeakisiwa katika maandiko ya kinabii.” (“Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu; adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” Is.53:4,5). Na sasa, Mungu wa milele amekwisha kutoa mamlaka ili kuifanya siri ijulikane kwa namna ambayo mataifa yote ya dunia watatambua jinsi ya kuishi (utii), ambako kunahimizwa na imani ya kusikia.” Rum.16:25,26). Hitimisho liko wazi; ilichukua kosa moja kuwahukumu wanadamu wote; tendo moja la haki linamtangazia mwanadamu yule yule kuwa hana hatia! Kutokutii kwa mtu mmoja kunawathibitishia wanadamu wote kuwa ni wenye dhambi; lakini utii wa mtu mwingine unawathibitishia wanadamu wote kuwa wao ni wenye haki! (Rum.5:18,19).
Kanuni ya imani ni kuona yale Mungu ayaonayo. Mungu huyataja yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.” (Rum.4:17). Hatuangalii mambo ambayo hisia zinatazama, bali tunaangalia ufunuo wa yasiyoonekana kana kwamba yamefunuliwa katika kioo cha Kristo ndani ya kila mtu. (2Kor.3:18; 4:18)
Ebr. 2:8 “Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake, hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini ya mtu.
Ebr. 2:9 Ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu.
Ebr. 2:10 Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso.
Ebr. 2:11 Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa, wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake.” (Tafsiri ya English Standard Version).
ORODHA YA VITABU
Maandiko ya Kigriki:
Textus Receptus
Robinson/Pierpont Bysantine
Westcott-Hort
Vitabu vya ufafanuzi:
Adam Clark
Albert Barnes
John Gill
Kamusi na Itifaki ya Biblia:
Strongs exhaustive concordance
J.H. Thayer Greek-English Lexicon
Walter Bauer’s Griechish-Deutches Worterbuch
www.mirrorreflection.net
fdt@mailbox.co.za
PO Box 1428
Hermanus South Africa 7200
Vitabu vingine vya mwandishi:
MUNGU ANAKUAMINI WEWE (Pia Ki-afrikaana, Ki-rusi, na Ki-venda)
ILITENDEKA! (Ki-afrikaana, ‘Kant en Klaar’)
KUMBATIO TAKATIFU (Ki-afrikaana INTIEM MET GOD)
SIRI IMEFUNULIWA (Ki-afrikaana, Ki-rusi)
JINSI YA UPENDO WAKE
SHANGWE YA URAFIKI
Kimetafsiriwa na:
Mch. Z.E.Mwalusambo
2008
Mirror Translation Copyright Francois du Toit 2007. All Rights Reserved. Used by permission.Online Parallel Bible